MFANYAKAZI WA NDANI ( HAUSIGELI) ADAIWA KUMUUA MWAJIRI WAKE KWA KUMCHOMA KISU SEHEMU YA TITI LA KULIA
Karani wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Asha Juma(24), ameuawa kwa kuchomwa kisu na mfanyakazi wake wa ndani.
Tukio hilo limetokea jana saa 4:00 asubuhi eneo la Sabasaba katika kata ya Utemini mjini Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema mauti
yalimfika karani huyo mara baada ya kuchomwa kisu sehemu ya titi la
kulia na mfanyakazi huyo wa ndani aitwaye Valetina Kerenge(17).
Msichana huyo ambaye ni mwenyeji wa mkoani Mwanza wilayani
Ukerewe, inasadikiwa alilifanya tukio hilo wakiwa ndani na baada ya
hapo alipata kiwewe na kukimbilia nje ya nyumba aliyokuwa akikaa na
kwenda kwa majirani kuomba msaada.
Inasemekana wakati juhudi za majirani za kunusuru uhai wake
zikifanyika ili kumuwahisha hospitali kwa matibabu, ghafla marehemu huyo
alianguka chini na kufariki papo hapo.
“Imesikitisha maana chanzo halisi hakijajulikana, maana msichana huyu alipoona mambo siyo alikimbia,” alisema Kamanda Kamwela.
Kamanda alisema tayari msako mkali wa polisi ulifanikisha kumpata
majira ya saa 8 mchana akiwa katika harakati za kutoroka maeneo ya
uwanja wa ndege.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida
kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi, na baada ya kuchunguza ndugu wa
marehemu watakabidhiwa kwa taratibu za kuusafirisha mwili huo kuelekea
mkoani Shinyanga kwa mazishi.
Jeshi la polisi linamshikilia msichana huyo kwa ajili ya mahojiano.
No comments