ads

Breaking News

Ebola imekuwa janga Afrika Magharibi



Zaidi ya vifo 450 vimetokana na Ebola huko Afrika Magharigi
Mawaziri wa afya 11 kutoka mataifa ya Afrika magharibi wanakutana mjini Accra, Ghana, kwa siku mbili ili kuzungumzia mkakati gani utumike kudhibiti kuenea kwa Ebola katika kanda hiyo.
Tayari visa vya ugonjwa huo vimepatikana katika nchi ya Guinea, Liberia na Sierra Leone, na shirika la afya duniani, WHO linasema kuwa hilo ndilo tukio kubwa zaidi la kusambaa kwa ugonjwa huo katika eneo kubwa.

Mkutano huo utazungumzia, tisho la hivi sasa la kuenea kwa ugonjwa huo.
Pia maelezo yatasikizwa kutoka kwa wagonjwa walionusurika, si tu kutoka Afrika magharibi, bali pia kutoka Uganda, taifa lililofaulu kupambana vilivyo na ugonjwa huo karibu miaka kumi iliyopita.
Viini vya ugonjwa hatari wa Ebola husambaa kwa kasi
 
Mkurupuko huo wa sasa tayari umewaua zaidi ya watu 450, wengi wao kutoka Guinea.
Mataifa mengine yanayotarajiwa kushiriki mkutano huo ni Ivory Coast, Mali, Guinea Bissau, Senegal, DRC na Gambia ambayo inasemekana kuwa katika hatari zaidi ya maambukizo hayo ya Ebola.
Ebola ni miongoni mwa magonjwa hatari sana duniani ambao hauna tiba kamilifu na vifo aghalabu hutokea muda mfupi baada ya maambukizo iwapo hamna mikakati kabambe ya kudhibiti athari zake kwa mgonjwa. Miongoni mwa athari hizo ni mgonjwa kuvuja damu na maambukizi hufanyika kwa kasi kutokana na majimaji ya mwilini ya mgonjwa kumpata mtu mwingine.
Katika hali hii ya sasa wataalam wanasema kuwa kuenea kwa ugonjwa huo kwatokana na unyanyapaa na uoga wa wagonjwa kutengwa huku visa vya wanafamilia kuwaficha wagonjwa wao vikiripotiwa.
Tayari Liberia na Sierra Leone wamonya kuwa yeyote atakayepatikana au kushukiwa kumficha mgonjwa wa Ebola, atashtakiwa.
Mikusanyiko na safari ya watu baina ya nchi pia kunatoa fursa kwa maradhi hayo kusambaa.
WHO tayari imewatuma wataalam zaidi ya 150, huko Afrika ya Magharibi, ili kusaidia kukabiliana na hali hiyo lakini wamesema kuwa utashi zaidi wa kisiasa unahitajika ili kupatikane suluhu la kudumu la kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

No comments