ISIS: Njooni mulijenge jimbo la kiislamu
Kiongozi wa kundi la wapiganaji wa kiislamu ISIS
limewataka waislamu waelekee Iraq na Syria kusaidia kulijenga jimbo
jipya la kiislamu.
Katika kanda ya sauti, Abu Bakr al-Baghdadi amewaomba waislamu wahamie katika 'jimbo la kiislamu' akieleza kwamba ni jukumu.Alitoa wito maalum kwa majaji, madaktari, wahandishi na watu walio na ujuzi wa kijeshi na uongozi.
Katika ujumbe wa awali wa kanda ya sauti, ISIS lilimtaja Abu Bakr al-Baghdadi kama khalifa, au kiongozi wa waislamu kote.
Ramadhan
Serikali kuu mjini Baghdad imeshindwa kudhibiti maeneo mengi kwa wanamgambo wa madhehebu ya kisunni, wakiongozwa na Isis katika mwezi uliopita.
Kundi hilo la wanamgambo wa kiislamu linasema jimbo lake litaenea kutoka Aleppo kaskazini mwa Syria hadi katika jimbo la Diyala mashariki mwa Iraq.
Kwa muda mrefu, wanajihadi wengi wametaka kuunda jimbo linaloongozwa kwa sheria za kiislamu.
"Kimbieni waislamu muje katika jimbo lenu. Hili ni jimbo lenu. Kimbieni muje kwa kuwa Syria sio ya raia wa Syria, na Iraq sio ya raia wa Iraq," al-Baghdadi alisema katika ujumbe kwenye kanda hiyo ya sauti siku ya Jumanne.
Aliwaomba pia wapiganaji kuongeza mapigano wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ulioanza siku ya Jumapili.
Sio mengi yanayojulikana kuhusu kiongozi huyo wa ISIS aliyepewa jina la utani, "shekhe asiyeonekana", ambaye tofauti na viongozi wa al-Qaeda kama vile Osama Bin Laden na Ayman al-Zawahiri, haonekani katika ujumbe wa kanda za video.
Katika ujumbe wake alitoa orodha ndefu ya nchi ambazo anasema waislamu wanakosewa - Kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati hadi Myanmar (inayofahamika pia kama Burma).
"kwa jina la MwenyeziMungu, tutalipiza kisasi! Hata kama itatuchukuwa muda, lakini tutalipiza kisasi," alisema.
Siku ya Jumanne, ISIS ilisema kwamba imedhibiti mji wa Syria, Boukamal, uliopo mpakani na Iraq. Kiongozi wa kundi hilo pia inasemekana aliwaachilia huru zaidi ya wafungwa 100 waliokuwa wanawazuia katika mji uliopo kaskazini mwa Syria, Al-Bab.
Picha ya pekee ya al-Baghdadi iliyotolewa na wizara ya ndani Iraq
No comments