Familia
moja ya Uturuki inawapasua kichwa wanasayansi, kutokana na wanandugu
watano kutokuwa na uwezo wa kutembea kama binadamu, na badala yake
wanatembea mithili ya wanyama, wakitumia miguu na mikono.
Hata
hivyo, katika uchunguzi wao wa awali, wanasayansi hao wameeleza kuwa,
hali iliyowakumba wanandugu hao haina uhusiano na mabadiliko ya
binadamu, kwamba wanaanza kurudi katika zama za mwanzo ambako inaelezwa
walitembea kwa miguu minne, wengine wakisema walianza kuwa nyani.
Ndugu
hao watano ambao ni kaka na madada, wakiwa na umri wa miaka 16 hadi 34
kutoka kijiji cha Jimbo la Hatay, kusini mwa Uturuki, walianza
kufuatiliwa na wanasayansi mwaka 2005 baada ya kugundulika na watu
kutoka nje ya kijiji chao.
Wanatembea kwa mtindo wa kutambaa kama
dubu kwa mikono na wanaweza kusimama tu kwa muda mfupi, kwa magoti yao.
Utafiti wa hivi karibuni ulifanywa na wanasayansi, Shapiro, Whitney
Cole, Scott Robinson na Karen Adolph, wote wa Chuo Kikuu cha New York,
Jessica Young wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Northeast Ohio na David
Raichlen, wa Chuo Kikuu cha Arizona.
“Lakini hawa hawana uhusiano na
mgeuko wa binadamu kwamba baada ya kupitia hatua kadhaa za mabadiliko,
sasa wanarudi katika hatua za awali, hilo halipo,” mmoja wa wanasayansi
hao amenukuliwa akisema.
Nadharia za awali zilidai familia ya Ulas
ilikuwa ikitembea kama nyani, na kupendekeza kuwa huenda ni hatua ya
kurudi nyuma kwa mabadiliko ya binadamu.
Lakini sasa, wanasayansi wa
Kimarekani wamethibitisha kwa kusema wanandugu hao wanakabiliwa na
kasoro isiyoonekana na hutokea mara chache.
Katika ripoti
iliyochapishwa na PLOS One, watafiti walisema familia hiyo wanatembea
kwa namna tofauti kama nyani, ambao wakitembea huweka mikono upande
mmoja na miguu upande mwingine wakijirudiarudia.
Walidai kutembea kwa wanandugu hao ni matokeo ya hali ya kurithi ambayo husababisha uwiano wa akili kutatizika.
“Nilikuwa
na hamu ya kuweka rekodi sawa, kwa kuwa haya madai ya asili na sababu
ya kutembea kama mnyama wa miguu minne imechapishwa mara kwa mara, bila
kuwepo uchambuzi wa kwa nini wanatembea hivyo, na watafiti ambao si
wataalamu wa namna mamalia wa hali ya juu wanavyotembea," Mtafiti
Kiongozi Liza Shapiro wa Chuo Kikuu cha Texas alilieleza gazeti la The
Washington Post.
“Tumeonesha wanyama wa miguu minne wanavyofanana na
mtu mzima mwenye afya njema ambaye ameambiwa atembee kwa miguu minne
wakati wa kufanya majaribio.
Mwaka 2005, watafiti wa Uingereza
walikubali katika utafiti tofauti kuwa utembeaji wa ndugu hao
unatofautiana na baadhi ya mamalia wengine, ikizingatiwa wenyewe hubeba
uzito wao wote kwenye viganja vya mkono na kifundo cha mkono na sio
kiungio.
Hata hivyo, Mtaalamu wa Bayolojia wa Uturuki, Uner Tan
awali alidai wanandugu hao, ambao pia wanaonekana kuwa wameathirika
kwenye ubongo wanakabiliwa na hali inayoitwa Uner Tan Syndrome.
Alisema
watu wanaokabiliwa na hali hiyo hutembea kwa miguu minne na mara
nyingine huzungumza kama wanyama na huwa na mtindio wa ubongo.
“Ghafla
nimegundua wanatembea kwa mtindo kama nyani kama walivyokuwa wahenga
wetu… nilikuwa wa kwanza kupendekeza kuwa kuna uwezekano wa hali ya
binadamu kugeuka na kurudi enzi za zamani za ubinadamu,” alisema.
Wandugu
hao ambao wazazi wao wanatembea kawaida, mara ya kwanza walirushwa
mwaka 2006 kwenye dokumentari ya BBC2, dokumentari hiyo ikiitwa The
Family That Walks On All Fours.
Wakati mabinti wawili na mtoto mmoja
wa kiume wamekuwa wakitembelea mikono miwili na miguu miwili, mtoto
mwingine wa kiume na kike mara nyingine huweza kutembea wakiwa
wamenyooka sawa, ingawa si kwa muda mrefu.
Profesa Nicholas
Humphrey, ambaye aliitembelea familia hiyo mara mbili wakati wa
dokumentari hiyo, alisema, “inashangaza kama mfano wa kitu cha ajabu cha
maendeleo ya binadamu. Lakini kinachovutia ni jinsia wanavyoweza kuishi
katika ulimwengu wa kisasa.”
Alisema alifikiri familia hiyo imerudi
katika silika ya mfumo wa tabia iliyojikita ndani sana kwenye ubongo,
lakini aliachwa wakati wa mageuko.
“Sidhani kama walitakiwa kuwa
wanyama wanaotembelea miguu minne kutokana na jeni zao, lakini mfumo wa
utengenezaji jeni zao zinawaruhusu kuwa hivyo,” alisema.
Wanandugu
hao watano ambao wana kaka na dada zao wengine 14 ambao hawajaathirika
na hali hiyo, hutumia muda mwingi kukaa nje ya nyumba yao ya familia
iliyoko kijijini.
Hata hivyo, mmoja wao hutembea kijijini, kuchanganyika na kuzungumza na watu.
No comments