ads

Breaking News

Nay wa Mitego adai alikuwa KIBAKA kabla ya kuwa Msanii..!!

ney
Kwa mara ya kwanza staa wa Bongo Fleva, Emanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ ameibuka na kuuelezea upande wa pili wa maisha yake kuwa kabla hajawa mwanamuziki alikuwa mwizi balaa!
 
Akizungumza na mwandishi wetu ana kwa ana jijini Dar es Salaam juzi, staa huyo alikiri kupitia katika majanga kibao maishani mwake likiwemo la kulala katika vituo mbalimbali vya polisi vya jijini Dar kufuatia kufanya matukio ya uhalifu.
 
“Kwanza kabisa nilikuwa nalala Feri na watoto machokoraa. Nilikuwa naona ndiyo maisha japokuwa nilijua kuna maisha mengine mazuri zaidi lakini ningeyapate?
 
“Dah! Yaani kusema kweli nilipita kwenye majanga makubwa sana jamani! Anyway, kimsingi ukweli wa maisha yangu siwezi kuuficha maana nitakuwa najiongopea bure kwani ni kweli niliishi katika maisha ya matukio sana,” alisema Nay.
 
Akizidi kutiririka , Nay ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa Mr Nay aliweka bayana kwamba kwa nyakati tofauti aliwahi kuiba  vitu mbalimbali (hakupenda kuvitaja) kwa watu wa karibu yake akiwemo Prodyuza Paul Mathysse ‘P Funk’ na kwenye studio moja iliyopo maeneo ya Mwenge jijini Dar.
 
“Enzi zangu nilikuwa balaa, Majani mwenyewe (P. Funk) nilishawahi kumliza, nakumbuka pia kuna jamaa zangu walikuwa na studio ya muziki pale Mwenge nao niliwapiga.
 
“Tena hawa jamaa wa studio nakumbuka walikuja kinitaiti nikiwa kwenye msiba, wakanitia pingu na kunipeleka kituo cha polisi lakini bahati nzuri marehemu John Mjema, alikuwa mshikaji wangu sana, akaja kunitoa,” alisema Nay.
 
John Mjema ‘Bomba la Mvua’ alikuwa mwanamuziki wa Kizazi Kipya, alifariki dunia Februari 10, 2008 kwa kujichoma kisu cha shingo nyumbani kwake Mtoni Kijichi jijini Dar.
 
Nay akaongeza: “Kulala polisi nadhani ni kama mara saba hivi na mara zote aliyekuwa akinitoa ni John Mjema. Yeye wakati ule alikuwa akifanya kazi kule maeneo ya Feri.”
 
Pamoja na matukio hayo ambayo Nay ameyafanya, alisema alishatubu na kumwomba Mungu amsamehe kwani anaamini ujana ndiyo ulikuwa ukimsumbua.
 
“Yaliyopita si ndwele, kwa sasa naganga yajayo maana muziki unanilipa na naendelea na harakati zangu kama kawaida, nilishasahau hayo matukio ya ajabuajabu,” alimaliza Nay.
 
Miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoyapata msanii huyo kupitia muziki wa Bongo Fleva ni kujenga nyumba Kimara-Rombo jijini Dar na gari la kutembelea aina ya Nissan Murano.

No comments